Naomba nianze kwa kuazima maneno ya Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar-es-salaam Ndugu, Alexander B. Makulilo kwenye moja ya makala yake kwenye gazeti la Mwananchi julai 23 2011, Taasisi yote ile kama ilivyo kwa chama cha siasa “huzaliwa, hukua, huzeeka na kufa kulingana na mazingira na mahitaji ya nyakati”. Hoja kuu ya Makulilo imelenga katika kuona vyama vya siasa kujitathmini kimfumo kuanzia itikadi, ambayo hutoa sura nzima ya muundo wa chama , malengo yake, maadili ya wanachama na viongozi wake na njia mwafaka za upatikanaji wa rasilimali kuendesha chama. Nimeanza kwa maneno haya kutoa tafakari yangu dhidi ya hoja za Mwanajamii mwenzangu anayejitambilisha kwa jina la Mkandara katika uzi wake “Waraka wa wazi kwa viongozi wa CHADEMA”
Awali ya yote napenda kumpongeza kwa kazi nzuri ya uchambuzi ambao umejaa mantiki ya hoja katika kutafakari na kujadili juu ya mustakabali wa nchi na kutazama kwa kina mwenendo wa siasa katika nchi yetu. Mwandishi ameazima maneno mawili, “do the right things” na “do things right” kuwasilisha kwa mapana mantiki wa hoja yake, nami naomba nielekeze fikra na mtazamo mbadala ambayo itatuwezesha kupanua zaidi wigo wa uelewa juu ya changamoto mbalimbali ambazo zitatusaidia kupima uhai na uhalali wa siasa zetu. Binafsi natazama CHADEMA kama chama ambacho kinakua hivyo bado kina nafasi ya kujitathmini na kuona ni kwa jinsi gani kinaweza kukabliana na changamoto mbalimbali katika kipindi hiki cha maandalizi ya kupewa mamlaka ya kuongoza nchi yetu na watu wake. Ukuaji wa CHADEMA unapitia katika vikwazo mbalimbali ambavyo bila umakini na ujasiri wa viongozi wake na uvumilivu wa wafuasi na wanachama wake chama hiki kinaweza kabisa kupoteza mwelekeo. Tofauti na binadamu mmoja mmoja ambapo vizingiti vya ukuaji wake husababisha kudumaa kimwili na kifikra, vizingiti hivi vina maana kubwa sana kwenye chama cha kisiasa ambacho kinakwenda kupewa mamlaka makubwa ya kuongoza nchi na watu wake.
Hoja ya Mabadiliko yapi ambayo CHADEMA inayaongoza ni jambo ambalo viongozi wa CHADEMA wanapaswa kuyapa kipaumbele ili hatimaye yaweze kuingia kwenye bongo za watanzania. Dr. Slaa aliwahi kutamka kwamba angependa kuongoza taifa kwa kufuata vipaumbele wakati wa uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, na moja ya kipaumbele ambacho CHADEMA inapaswa kuyatekeleza sasa kwa ufanisi mkubwa ni kuwaeleza watanzania ni kwa vipi na kwa namna gani chama kinaenda kuyasimamia yale ambayo wanayoita mabadiliko na hatimaye kuleta matokeo chanya kwa Watanzania na huu ndio utakuwa kianzio (turn point) kutimiza ndoto za mabadiliko ya kiuongozi na kimfumo katika nchi yetu.Watanzania wanapaswa kuelezwa na kuelewa kwamba kinachopingwa si viongozi tu wa CCM bali ni sera zao ambazo hazina tija kwa taifa letu. Na wanaopingwa lazima watambue kwamba wanaopingwa sio wao tu bali ni hoja na sera zao. Lazima Watanzania tuanze kujifunza umuhimu wa kuwekeza katika siasa za akili kufuatana na ujuzi halisi na hali ya mazingira yetu. Hapa naungana kabisa na hoja ya Mkandara.
Zoezi la kutafuta wanachama kupitia operesheni za chama ni jambo la muhimu katika kujenga misingi madhubuti ya chama kama taasisi imara inayoongozwa na watu wenye weledi wa kutosha kuongoza nchi. Chama chochote makini cha siasa lazima kiwe mkakati na mtaji wa wanachama ambao watakuwa mstari wa mbele kuongoza mabadiliko na kutafsiri kwa lugha fasaha matarajio ya mabadiliko hayo. Siku zote ukienda vitani lazima uandae silaha ili kusambaratisha ngome ya mpinzani, vivyo hivyo ukiwa na kikosi imara katika mchezo wa soka lazima ufanye maandalizi ya kikosi mbadala. Kukuza mtaji wa wanachama ni moja ya silaha muhimu ya kuongoza harakati za mabadiliko. Umaridadi wa kutandaza soka na kufunga magoli ndio chimbuko la kuongezeka kwa mashabiki hivyo ndivyo ilivyo kwa chama cha siasa katika kuongeza mtaji wa wanachama.
Huwezi kutenganisha siasa za ukanda, ukabila na udini bila kutaja Chama Cha Mapinduzi kama moja ya chanzo kikuu cha kujengeka kwa hisia hizi nchini kwetu. Na hili ni zao la kuwekeza siasa dhaifu ambazo zimejengeka katika kucheza na hisia za ndani za watu. Toka kuanza kwa mfumo wa vyama vingi CCM imeshindwa kujitathmini kisera, kimuundo na kiutendaji, kukubaliana na mabadiliko makubwa na kujikuta ikingia katika siasa za ushindani kwa kutumia njia za haramu (udini, ukabila na ukanda) kupasua ngome ya mpinzani. Na hivyo kupotosha dhana halisi ya demokrasia katika kuwekeza katika siasa za akili zilizojaa busara, ujuzi na maarifa. Hisia hizi ndizo ambazo zinachipuka kwa kasi ndani ya taifa letu. CHADEMA ni chama kinachokuwa hivyo lazima kipitie katika kipindi cha mpito, kuasisiwa na mchaga si hoja ya kusema kwamba chama hiki ni chama cha wachaga la hasha, CHADEMA kama chama ya kisiasa lazima itakumbana na mabadiliko ya kiuongozi ndani ya chama ambayo yatajenga taswira ya kitaifa, ikipingana na mabadiliko ni dhahiri migogoro ndani ya chama itajengeka na hivyo kupoteza mwelekeo.
Naomba nihitimishe tafakari yangu kwa kuandika maneno yafuatayo; nchi yetu inapita katika kipindi cha mpito kuelekea mabadiliko makubwa ya kisiasa ambacho tusipokuwa makini AMANI yetu itapotea. Suala la msingi tujiulize ni nani tavunja amani ndani ya tifa letu? Ni serikali ya CCM, CHADEMA au CUF? Je tumeridhia mfumo wa vyama vingi kama mtindo (model) kuwafurahisha wajomba na mashangazi wetu wa mataifa ya nje au kuimarisha demokrasia ndani ya taifa letu? Je vyombo vinavyosimamia haki na usalama wa nchi viko tayari kulinda demokrasia tuliyoridhia kwa utu, usawa na haki kamili? Ni dhahiri kwamba nguvu, ubabe na vitisho utapeleka taifa letu mahali kwenye machafuko.
Home »
» Waraka wa wazi kwa viongozi wa CHADEMA”
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !